
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Anthony Mtaka, amesema wananchi wa mkoa huo wanajivunia mafanikio ya maendeleo, hususan ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mkoani humo, uliogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 20, kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Amesema uwekezaji huo umeongeza fursa za elimu ya juu kwa vijana wa Njombe na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hivyo kuwapa nafasi ya kutimiza ndoto zao za kitaaluma.

Mhe. Mtaka amesema hayo katika Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Mei Mosi yaliyofanyika mkoani humo, akisisitiza kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametimiza ahadi ya kuanzisha Chuo Kikuu mkoani humo, akieleza kuwa ndoto ya muda mrefu ya wazee sasa imetimia na tayari mchakato wa udahili umeanza.

Ameongeza kuwa mkoa huo unaendelea kunufaika na juhudi za Serikali katika sekta mbalimbali, ikiwemo ajira, ambapo idadi kubwa ya walimu wameajiriwa, hatua inayochochea maendeleo ya elimu na huduma kwa jamii.


