Serikali ya Tanzania imeendelea kuonesha dhamira ya kuwezesha vijana wa Kitanzania kupata elimu ya juu katika fani za Sayansi ya Data, Akili Unde na Sayansi Shirikishi kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended DS/AI+.



Katika kikao maalum kilichofanyika Septemba 28,2025 katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Arusha, Viongozi wa Wizara na Kamati inayoratibu mpango huo wamefanya tathmini ya awali ya maandalizi na maendeleo ya wanufaika walipo katika Kambi Maalum ya Maarifa.



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi amesema Serikali itahakikisha wanufaika wanapata elimu bora kuijenga Tanzania yenye rasilimali watu wenye ujuzi katika Sayansi na Teknolojia sambamba na kukuza uwezo wa taifa kushiriki kikamilifu katika mapinduzi ya nne ya viwanda na uchumi wa kidijitali.



Makamu Mkuu wa Taasisi ya NM-AIST, Prof. Maulilio amesema Taasisi hiyo inaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara kuhakikisha wanufaika wanapata maarifa ya kiwango cha juu na mafunzo ya vitendo kuwawezesha kuwa tayari kuingia katika Vyuo Vikuu Mahiri Duniani.