
Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Fredrick Salukele, amesema kuwa Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia katika shule za amali na vyuo vya ufundi nchini.

Ameeleza kuwa kuna mipango miwili mikuu inayotekelezwa kwa lengo hilo. Mpango wa kwanza unahusisha Mradi wa Education Skills for Productive Jobs - Awamu ya Pili, ambapo Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kufundishia kwa shule za amali 103 zinazijengwa, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) 54, pamoja na Vyuo vya VETA 65 vinavyojengwa na vyuo 25 vya vilivyokamilika.

Mpango wa pili unatekelezwa kupitia bajeti ya Wizara, ambapo fedha zimetengwa kwa ajili ya kununua vifaa vya kufundishia katika shule za sekondari pamoja na shule 29 za ufundi. Kwa ujumla, takriban shilingi bilioni 39 zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.

Dkt. Salukele amesema hatua hizi ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, ili kuongeza ujuzi na maarifa kwa wanafunzi wanaosomea fani mbalimbali za ufundi stadi.

