Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amekutana Kiongozi wa Kampuni ya Empower Limited Miranda Naiman na kujadili juu ya utekelezaji wa mitaala mipya na mipango na mikakati ya kuboresha elimu ya juu nchini.



Kikao hicho kimefanyika Machi 08, 2024 Jijini Dar es Saalaam ambapo Katibu Mkuu huyo amemweleza Kiongozi wa Empower kuwa Serikali imeweka mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuboresha elimu nchini kuanzia ngazi ya elimumsingi hadi elimu ya juu.



Ameongeza kuwa mageuzi yaliyofanyika katika ngazi ya elimumsingi yanakwenda mpaka elimu ya juu ili kuwezesha mifumo yote ya elimu nchini izungumze kwa pamoja kwani mabadiliko yaliyofanyika lazima yafanyike na ngazi ya elimu ya juu na maeneo mengine ya elimu.



"Tumeona pengo katika mtalaa wetu wa elimumsingi, na wizara imefanya maboresho ya mitalaa ili iweze kuendana viwango vya ubora wa kimataifa kwa kuzalisha nguvu kazi inayokidhi viwango na uwezo wa mahitaji katika soko letu la sasa na la Duniani” amesema Katibu Mkuu huyo.



Aidha, Prof. Nombo ametoaa wito kwa taasisi za elimu ya juu kuanzisha programu za kuwawezesha wanafunzi kuchagua kozi sahihi zilizopo katika soko wanapokuwa chuoni ili ziweze kuwasaidia wanapohitimu kwa kujiajiri ama kupata ajira kwa haraka.



Katibu Mkuu huyo ameipongeza Kampuni ya Empower kupitia ya Generation Empower yenye lengo la kutoa mafunzo katika stadi za karne ya 21 ambazo ni ujasiliamali na uelewa wa soko la ajira katika sekta mbalimbali.



Kiongozi wa Kampuni ya Empowe Miranda Naiman amemweleza Prof. Nombo kuwa Kampuni ina programu ya kuwaendeleza vijana, kujenga daraja kati ya Sekta ya Umma na Binafsi, kubadilisha mitazamo, kuandaa vijana wa Kitanzania kwa mustakabali wenye ushindani, na kukuza kizazi cha wabunifu wenye uwezo wa kutatua matatizo katika jamii.

“Programu yetu ni jumuishi kabisa ya jukumu la kijamii la kampuni yetu kwani tunaona hitaji la kuunga mkono uwezo wa vijana katika sekta ya elimu ya Tanzania, tunataka kuwa na ushirikiano na wizara ili kuweza kuongeza matokeo makubwa ya programme hii katika elimu ya ngazi za juu”. Amesema Naiman