Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameipongeza Bank ya KCB Tanzania kwa namna inavyowezesha vijana kupata mafunzo ya Amali kupitia program ya Tujiari.

Akizungumza jijini Dodoma na wawakilishi wa KCB waliofika kuzungumzia programu hiyo, Waziri Mkenda amesema jitihada zinazofanyika na Benki hiyo zinaunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha vijana wanapata ujuzi.Amesema mafunzo ya amali ni muhimu sana na kwamba vijana wana kiu kubwa ya kupata mafunzo hayo kwa kuwa yanamuandaa kijana kujiajiri au kuajiriwa.

“Mnachofanya KCB kinatupa picha kubwa ya kile ambacho Rais amelekeza, kuongeza fursa ya mafunzo ya amali, tunaahidi tutafanya nanyi kazi, tunataka tushirikiane katika kuwafuatilia vijana wanapomaliza mafunzo na juhudi mnazowasaidia kujiajiri ili kuona mafanikio yakoje na nini tunaweza kufanya katika mitaala yetu ili kuboresha,” amesema Prof. Mkenda

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Carolyne Nombo ameishukuru Benki ya KCB Tanzania kwa ushirikiano ambao wameonesha kwa Serikali kwa kuwasaidia vijana kupata ujuzi.

“Niwasihii vijana ambao mtakwenda kusoma kupitia program ya Tujiajiri inayotolewa na Benki ya KCB Tanzania kuwa makini na mafunzo haya kwa kuwa yatawasaidia kusimama kama kijana wa kitanzania kutengeza maisha yenu na kuwa na mchango katika maendeleo ya Taifa”, amesema Prof. NomboAkizungumzia Programu ya Tujiajiri inayotolewa na Benki ya KCB Tanzania Mkuu wa Idara ya Masoko, Mawasiliano, Uhusiano na Maendeleo ya Jamii ya Benki hiyo Christina Manyenye amesema Program hiyo ilianza mwaka 2016 na kwamba ina lengo la kubadilisha mawazo ya kijana wa kitanzania kuacha kufikiria kuajiriwa na badala yake afikirie kujiajiri.

Amesema program hii ni endelevu na kwamba inawafadhili vijana asilimia 100 ya ada, vitendea kazi, mavazi yanayotumika kwenye mafunzo kwa vitendo na kwamba baada ya kuhitimu masomo yao wanaendelea kuwafuatilia katika biashara zao kama walezi kwa kuwapa ushauri na wakati mwingine mitaji.

" Mwaka huu tutawezesha mafunzo kwa vijana 5000 kupitia VETA Tanzania Bara na Zanzibar. Baadhi ya Mikoa nufaika Tanzania bara ni Dar es Salaam, Mwanza, Arusha Morogoro Kilimanjaro na Geita,”amesema