Timu ya kitaifa ya utekelezaji wa mradi wa kuimarisha Ufundishaji na Ujifunzaji kwa shule za Awali na Msingi Tanzania (BOOST) imeridhishwa na ujenzi wa miundombinu katika shule baada ya kutembelea na kujionea ubora na matokeo ya utekelezaji wa mradi huo katika kuongeza hamasa ya uandikishaji na ujifunzaji mkoani Mara.


 
Akizungumza katika ziara hiyo ya ufuatiliaji Mratibu wa mradi wa BOOST Lawrence Mselenga amesema Mkoa wa Mara umepokea zaidi ya bilioni 12.7 katika utekelezaji wa ujenzi wa shule mpya saba , vyumba 113, nyumba za walimu na vyumba vya madarasa ya elimu awali 18 ambapo mkoa huo umetekeleza afua zote.



Ameongeza kuwa afua hizo zinalenga katika kuboresha miundombinu, kuwajengea uwezo walimu na kulinda usalama wa wanafunzi.



Mselenga amesema moja ya matokeo chanya ya mradi ni ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi elimu ya Awali na Msingi.


 
Akizungumzia ziara amesema “tumefika kuona utekekezaji wa afua hizi kwa pamoja na wenzetu kutoka Benki ya Dunia na tumeridhishwa na utekelezaji. ” Lawrence Mselenga



Naye kwa upande wake Mtaalum wa masuala ya Elimu kutoka Benki ya Dunia Gemma Nifasha amesema wameridhika na utekelezaji katika shule zote walizotembelea na kuwa zinawawezesha wanafunzi kujifunza kwa haraka pamoja na afua ya walimu wenyewe kuwezeshana na kukumbushana majukumu yao ambayo ni moja ya afua katika utekelezaji ndani ya mradi wa BOOST hivyo ni jambo la kupongezwa na kujivunia kwa kile ambacho wanakitoa kinaleta tija kwa wanafunzi.



Nae mratibu wa mradi wa BOOST Mkoa wa Mara amesema pamoja na miundo mbinu kupitia mradi wametekekeza afua ya mafunzo kwa walimu wa darasa la tatu, nne, tano na la sita kuhusu mbinu za ufundishaji.



Timu hiyo ya ufuatiliaji inajumuisha watekelezaji kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, OR TAMISEMI na benki ya dunia imetembelea shule ya msingi Bukanga, shule ya msingi Mwisenge B na shule ya msingi Kiara katika manispaa ya Musoma mkoani Mara.