Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina jukumu la kusimamia na kuratibu utoaji wa elimu nchini kwa kuandaa sera, sheria na miongozo mbalimbali kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi elimu ya juu. Aidha, Wizara ina wajibu wa kusimamia na kuratibu maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu pamoja na matumizi yake katika sekta mbalimbali zikiwemo biashara, viwanda, kilimo na maisha ya kila siku kwa ujumla.
Kuhusu Wizara
MAJUKUMU
- Kwa mujibu wa Hati Idhini iliyotolewa tarehe 19 Disemba 2025, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza majukumu yafuatayo:
- 1. Kutunga na kutekeleza sera za elimu, sayansi, utafiti, huduma za maktaba, teknolojia, ubunifu na maendeleo ya mafunzo ya ufundi.
- 2. Kuendeleza elimu msingi kupitia utoaji wa ithibati ya mafunzo ya ualimu pamoja na maendeleo ya kitaalamu ya walimu.
- 3. Kubaini vipaji na kuviendeleza.
- 4. Kusimamia maendeleo ya mafunzo katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.
- 5. Kusimamia mfumo wa tuzo wa taifa.
- 6. Kuainisha mahitaji ya nchi katika ujuzi na kuyaendeleza.
- 7. Kuweka viwango vya taaluma ya ualimu.
- 8. Kusimamia ithibati na uthibiti wa shule.
- 9. Kusimamia huduma za machapisho ya kielimu.
- 10. Kuimarisha matumizi ya sayansi, uhandisi, teknolojia na hisabati (STEM).
- 11. Kuendeleza wataalamu wa ndani katika sayansi, teknolojia na ubunifu.
- 12. Kusimamia utafiti katika sayansi na teknolojia.
- 13. Kuendeleza rasilimali watu na kuongeza tija kwa watumishi walio chini ya Wizara.
- 14. Kuratibu shughuli za idara, mashirika, wakala, programu na miradi iliyo chini ya Wizara.
MALENGO
- Ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imejiwekea malengo yafuatayo:
- 1. Kuongeza fursa na ubora wa elimu na mafunzo katika ngazi zote.
- 2. Kutunga na kutekeleza sera za elimu, utafiti, huduma za maktaba, sayansi, teknolojia, ubunifu na maendeleo ya mafunzo ya ufundi.
- 3. Kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika elimu, sayansi na teknolojia.
- 4. Kuratibu na kuimarisha maendeleo ya utafiti na ubunifu kwa ajili ya kukuza uchumi wa jamii na maendeleo ya viwanda.
- 5. Kuongeza matumizi, mafunzo na kuweka kanuni za matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.
- Kukusanya rasilimali fedha na kuongeza uwekezaji katika elimu, sayansi, teknolojia, ubunifu pamoja na miundombinu.
- 6. Kuimarisha usimamizi wa taarifa katika sekta ya elimu pamoja na ujifunzaji wa kielektroniki (e-learning).
- 7. Kuimarisha mazingira ya kazi ili kuongeza tija na ufanisi katika utoaji wa huduma.
- 8. Kushughulikia masuala mtambuka katika sekta ya elimu.