
Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazingatia elimu jumuishi na yenye ubora stahiki.

Dkt. Mtahabwa ameeleza hayo Januari 05, 2026 jijini Dodoma akizungumza katika Hafla ya Uzinduzi na Ugawaji wa Magari na Vifaa vya Kidigitali vya Kielimu na Saidizi kwa Walimu, Wakufunzi na Walimu Tarajali wenye ulemavu nchini.

Kamishma huyo, amesisitiza kuwa elimu ni walimu, na walimu wa Karne ya 21, wasiwe hodari wa kushika chaki pekee, lazima wajue matumizi ya teknolojia na watumie kikamilifu katika ufundishaji na ujifunzaji.

"Vifaa hivi vya kidigiti vitajenga hadhi na kuwawezesha walimu wetu kutumia teknolojia kikamilifu katika kufundisha na kujifunza" amesema Kamishna wa Elimu.

