Serikali inaendelea kutekeleza afua mbalimbali ikiwemo kuondoa vikwazo vya kupata elimu kwa kutolewa kwa elimu ya msingi bila ada, kuifanya elimu ya lazima kuwa miaka 10, kutekeleza programu zenye lengo la kuwafikia Watanzania waliokosa fursa za elimu.



Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga Feberuari 02, 2024 Bungeni wakati akijibu swali Mhe Taska Restituta Mbogo (Viti Maalum) aliyetaka kufahamu mikakati ya Serikali ya kuhakikisha watanzania wote wanajua kusoma na kuandika ambapo ameongeza kuwa mikakati hiyo ni Elimu ya Watu Wazima na ujifunzaji endelevu, utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kisomo pamoja na kutoa fursa kwa wanafunzi walioacha masomo kwa sababu mbalimbali kurudi shuleni na kuendelea na masomo (re-entry program) kupitia Waraka Na. 2 wa mwaka 2021



Mhe. Kipanga ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma za maktaba nchini katika ngazi za Mikoa, Wilaya na shule ikiwa ni pamoja na maktaba mtandao ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi katika maeneo mbalimbali kupata huduma ya kujisomea huko waliko na kwamba itaendelea kuboresha miundombinu ya Taasisi ya Elimu ya Wazima kwa lengo la kuongeza fursa kwa Watanzania wengi zaidi kujiunga na Elimu ya Watu Wazima.



Naibu Waziri huyo amesema kulingana na Ripoti iliyotolewa na NBS, kwa sensa ya 2022 Tanzania imefikia kiwango cha 83% cha kujua kusoma na kuandika miongoni mwa watu wazima yaani miaka 15 na kuendelea ikiwa ni ongezeko la 6.3% toka 78.1% cha sensa ya 2012