
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza kuboresha Rasimu ya Kiunzi cha Uandaaji, Uchapaji, Uzalishaji, Usambazaji, Uhifadhi, Utunzaji na Matumizi ya Vitabu vya Kiada nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao maalum kilichofanyika Morogoro, Novemba 18, 2025 kwa niaba ya Kamishna wa Elimu, Dkt. Joyce Sigalla, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Uendelezaji Sera Elimu ya Msingi alisema hatua hiyo ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayoendelea katika sekta ya elimu. Mageuzi hayo yanajumuisha Maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014 (Toleo la 2023), Mabadiliko ya Mitaala ya Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari, pamoja na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP III 2025/26–2029/30).

Dkt. Sigalla alieleza kuwa lengo kuu ni kujadili na kuboresha rasimu ya kiunzi kitakachoweka mfumo mmoja wa kitaifa katika mnyororo mzima wa kitabu, kuanzia uandishi na uhakiki wa kitaaluma hadi usambazaji, utunzaji na matumizi shuleni.

Aidha, kikao hicho kimekusanya wadau muhimu kutoka TAMISEMI, Taasisi ya Elimu Tanzania, Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya, sekta binafsi na taasisi nyingine ili kuhakikisha mfumo unaojadiliwa una uhalisia, unatekelezeka, na unaweza kutatua changamoto zilizopo.


