
Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imetoa vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya jumla ya Sh. 769,390,000 kwa shule za Msingi na Sekondari 19 zilizopo katika mikoa 9 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Vifaa hivyo vinajumuisha madarasa janja, mbao janja, vishikwambi na kompyuta ambavyo vitawezesha ujifunzaji kwa wanafunzi hususan katika masomo ya sayansi na teknolojia, huku walimu wakinufaika kwa kutumia mbinu bunifu za ufundishaji na mifumo ya kidijitali kufuatilia maendeleo ya wanafunzi kwa ufanisi zaidi.

Hafla ya ugawaji wa vifaa hivyo imefanyika Machi 30, 2026 jijini Dodoma, ambapo Naibu Waziri wa Elimu, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuendeleza mageuzi makubwa katika sekta ya elimu kupitia matumizi ya teknolojia za kidijitali.

Amesema mageuzi hayo yanalenga kuboresha elimu kwa kuimarisha elimu ya lazima ya miaka 10, kuendeleza mkondo wa elimu ya Amali na kuimarisha mafunzo ya ualimu hususan katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).

"Leo tumegawa vifaa hivi, niombe visifungiwe kabatini, vitunzeni vitumike kwa muda mrefu na kuwanufaisha Wanafunzi wengi," amesisitiza Mhe. Wanu

Mhe. Wanu ameishukuru Lyra Organisation in Africa pamoja na wadau wengine wa sekta binafsi kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha matumizi ya teknolojia katika elimu. Amehimiza ushirikiano huo uendelee ili kujenga mfumo wa elimu wa kisasa na jumuishi unaotumia teknolojia kwa ufanisi.

Aidha, amewataka walimu, wanafunzi na wadau wote kutumia na kutunza vifaa hivyo ipasavyo ili viweze kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.


