
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, leo Agosti 07, 2025 Jijini Dodoma amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa India nchini Tanzania, Mhe. Bishwadip Dey ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya Elimu na namna ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja za sayansi na teknolojia.
Prof. Nombo amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kwa kutoa ufadhili wa masomo katika fani mbalimbali za kimkakati kama vile nishati ya nyuklia, tiba na sayansi ya data.
Ameeleza kuwa ufadhili katika fani hizo umekuwa chachu ya maendeleo ya rasilimali watu kwa kutoa nafasi kwa vijana kupata elimu bora katika maeneo yenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.
Aidha, viongozi hao wamegusia fursa za mafunzo ya ufundi stadi kwa Watanzania nchini India, ikiwa ni sehemu ya kuandaa wataalamu wa fani mbalimbali watakaosaidia katika kuharakisha maendeleo ya taifa wanaporudi nyumbani wakiwa na ujuzi unaokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.
Mhe. Balozi Bishwadip Dey ameipongeza serikali kwa kuendelea kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu katika ngazi mbalimbali za elimu.
Amesema kuwa Serikali ya India itaendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo katika sekta ya elimu nchini.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo, Prof. Daniel Mushi, amemshukuru Mhe. Bishwadip Dey pamoja na Serikali ya nchi hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuhakikisha watanzania wanapata elimu bora.