Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza kuanza rasmi kwa hatua ya utekelezaji wenye matokeo katika Mpango wa (Partnership Compact), ikiwa ni ishara ya mabadiliko kutoka mipango kwenda vitendo vinavyolenga kuboresha matokeo ya ujifunzaji kwa wanafunzi wote nchini.



Akizungumza Aprili 30, 2026 wakati wa ufunguzi wa kikao cha kwanza cha robo mwaka cha wadau wa mpango huo jijini Arusha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Mohamed Hussein Omar, amesema kikao hicho ni hatua muhimu katika kuhakikisha kunakuwa na uwajibikaji wa pamoja na utekelezaji unaolenga matokeo.



Amesema kuwa mpango wa (Partnership Compact) unatoa mwongozo wa pamoja wa kuboresha elimu ya msingi nchini, ukiwa na lengo la kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu jumuishi yenye ubora na inayozingatia matokeo ya ujifunzaji.



Dkt, Omar amefafanua kuwa katika kipindi cha siku mbili za kikao hicho, wadau wamejadili maendeleo yaliyofikiwa katika maeneo manne ya kipaumbele ya mageuzi ya elimu, ambayo yanahusisha masuala ya walimu, miundombinu, mifumo ya takwimu na ujumuishaji wa wanafunzi.



Aidha Dkt. Omar ametaja baadhi ya mafanikio kuwa ni pamoja na uboreshwaji mfumo wa upangaji wa walimu, ujenzi wa miundombinu ya shule, pamoja na kuimarishwa kwa mifumo ya ukusanyaji na matumizi ya takwimu.