
Tarehe 26 Machi, 2026 Mhe.Wanu Hafidh Ameir (Mb), Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia alitembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Afrika Kusini na kukutana na Watumishi wa Ubalozi pamoja na Wanafunzi wa Kitanzania wanaosoma Kozi mbalimbali katika Vyuo Vikuu vilivyopo jijini Johannesburg na Pretoria.

Katika Mkutano huo, Mhe. Ameir (Mb) alieleza hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kuboresha mazingira ya elimu na kujifunza nchini Tanzania. Hatua hizo ni pamoja na maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023; kuimarisha na kuongeza miundombinu ya elimu; kukuza matumizi ya teknolojia katika ufundishaji, pamoja na kuongeza fursa za elimu ya juu ndani na nje ya nchi.

Alisisitiza kuwa juhudi hizo zinaendana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025–2030 pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, inayolenga kujenga rasilimaliwatu yenye ujuzi, maarifa na ubunifu.
Baada ya mawasilisho hayo, Diaspora Wanafunzi walipata fursa ya kuuliza maswali, kutoa maoni na ushauri, pamoja na kueleza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika safari yao ya kielimu. Serikali, kupitia Wizara na kwa kushirikiana na Ubalozi, ilitoa majibu kwa changamoto zilizohitaji kushughulikiwa mara moja na kuahidi kuzifanyia kazi changamoto zitakazohitaji ufuatiliaji zaidi.

Mhe. Ameir (Mb) amehitimisha Ziara yake ya Kikazi nchini Afrika Kusini na leo tarehe 28 Machi, 2026 amerejea nchini Tanzania kuendelea na majukumu mengine ya Ujenzi wa Taifa.

