Katibu Mkuu wa Wizarau ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, ametoa wito kwa wadau wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unakuwa wa ubunifu, shirikishi, na wenye tija ili kuchangia kikamilifu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, katika sekta ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.



Akizungumza Agosti 11, 2025 jijini Dodoma, wakati wa Kikao cha Kamati Tendaji ya Mradi wa HEET, Prof. Nombo ameeleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo inaitaka Wizara kuandaa rasilimaliwatu yenye maarifa, ujuzi, na uwezo wa kuchochea maendeleo ya Taifa.



Amesisitiza kuwa Mradi wa HEET unapaswa kuimarisha miundombinu ya elimu ya juu, kuendeleza programu za amali, na kuongeza matumizi ya TEHAMA ili kuwajengea wahitimu uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisasa.



Katika kikao hicho, Prof. Nombo amekabidhi vishikwambi kwa wajumbe wa Kamati Tendaji ya Mradi kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kazi, huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi madhubuti, uwajibikaji, na matumizi bora ya rasilimali za umma.



Aidha, amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya Wizara, Taasisi za Elimu ya Juu zinazotekeleza Mradi, na wadau wa maendeleo, ili kuhakikisha kuwa Mradi HEET unatoa mchango wa moja kwa moja katika kukuza ajira, kuendeleza ubunifu, na kuimarisha maendeleo ya viwanda nchini.