Zaidi ya walimu 400 wa masomo ya Sayansi na Kingereza wa Shule za Msingi za Mkoa wa Morogoro katika manispaa ya Morogoro wameanza mafunzo ya siku mbili katika Kituo cha Shule ya Msingi Kikundi ya kuendelea kutekeleza mtaala ulioboreshwa.



Mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo yanayoendelea kufanyika nchi nzima katika maeneo mbalimbali kwa walimu wote ili kuwawezesha kupata uelewa wa pamoja juu ya mitaala iliyofanyiwa maboresho.



Afisa elimu wa Taaluma wa mkoa wa Morogoro, Bwana Wiliam Mapunda akizungumza kwenye mafunzo hayo amewaasa walimu wanaohudhuria mafunzo kuwa wasikuvu na kuelewa wanacho fundishwa ili kupata ujuzi utakaowasaidia katika maeneo yao ya ufundishaji.



"Nawaomba sana muwe wasikivu, muelewe mnapofundishwa na mkitoka hapa mkawafundishe pia walimu wengine ambao hawajapata nafasi ya mafunzo haya mkawajenge kupitia mewaka na Jumuiya za Kujifunza(JZK)" amesema Bwana. Mapunda.



Kwa upande wake, Mratibu wa mafunzo haya kutoka TET Bi. Elizabeth Macha amesema kuwa walimu wanaohudhuria mafunzo hayo watajengewa uelewa wa namna ya kutekeleza maudhui mapya katika masomo ya Sayansi na Kingereza.