
Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuongeza wigo wa ushirikiano na wadau mbalimbali wa elimu hatua ambayo imeimarisha mahusiano na kuchochea utekelezaji wa kazi mbalimbali.

Bi. Makala amesema hayo Novemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya Uzinduzi wa Mpango wa utekelezaji Mwongozo wa kuwarejesha Shuleni Wanafunzi waliokatiza masomo katika Elimu ya Msingi na Sekondari.

"Ushirikiano huu, umetusaidia kutumia vema rasilimali zinazopatikana kutekeleza mikakati mbalimbali kuwezesha elimu bora kwa watoto wetu" amesema Makala.

Aidha Mratibu huyo ameishukuru Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuitambua TEN/MET na kuipa jukumu la kuratibu uuandaaji wa mpango huo muhimu kwa Taifa.


