Hafla ya Nne ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kufanyika tarehe 13 Aprili 2026 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Super Dome.



Akizungumza jijini Dodoma Aprili 8, 2026 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema hafla hii hufanyika kila mwaka kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na kutambua mchango wake katika kukuza lugha ya Kiswahili na utamaduni wa Taifa.



Ameeleza kuwa Mwaka huu, mashindano yamehusisha nyanja nne za fasihi riwaya, hadithi za watoto, tamthiliya na ushairi.

"Tunaendelea kukuza kiswahili, kuendeleza vipaji vya uandishi bunifu, kulinda historia na utamaduni wa Taifa, pamoja na kuongeza hifadhi ya vitabu katika maktaba ndio malengo ya tuzo hii, amesema Prof. Mkenda



Amesema mgeni rasmi wa hafla hiyo atakuwa mshairi maarufu duniani Abdilatif Abdallah, mwenye asili ya Afrika Mashariki, ambaye aliwahi kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 15.

Hafla hiyo itatanguliwa na mjadala wa kitaaluma utakaoshirikisha waandishi bunifu wa Tanzania pamoja na wageni mashuhuri kutoka Uganda na Rwanda.



Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza zaidi ya shilingi milioni 800 katika kuchapisha na kusambaza vitabu vilivyoshinda tuzo, hatua inayolenga kuhamasisha usomaji na kukuza sekta ya uchapishaji nchini.

Tangu kuanzishwa kwake, Watanzania 27 wameshinda tuzo hii, huku washiriki wakiwa ni watanzania wakitoka ndani na nje ya nchi, ikiwemo Kenya, Jamhuri ya Czech na Australia.