
Wiki ya kongamano la ujifunzaji Kidijitali inayoendeshwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuhusu Elimu kiditali (Digital Learning Week 2025) inafanyika katika Makao Makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa, ikiwa na Kaulimbiu “AI's Transformative role in reshaping Education" ikilenga kuona Akili Unde na Mustakabali wake katika Mabadiliko ya kielimu Duniani.
Tukio hili la kimataifa linaleta pamoja viongozi wa elimu, wataalamu wa teknolojia, watunga sera kutoka mashirika ya kimataifa, serikali, Vyuo Vikuu, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi. Lengo kuu ni kuchochea mjadala wa kisera, kujifunza kwa pamoja, na kuunda mwelekeo mpya wa matumizi ya Akili Unde katika elimu kwa njia jumuishi, yenye kujali maadili na inayolenga kuleta maendeleo.
Tanzania, inawakilishwa na wajumbe mbalimbali wakuongozwa na Prof. Carolyne Nombo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST), na Dr. Alcardo Alex Barakabitze, Mratibu wa Teknolojia za kielimu (EdTech) kutoka Wizara hiyo.
Tanzania imechukua hatua madhubuti katika kuhimiza matumizi ya AI kwa njia salama na jumuishi ambapo mnamo Februari 2025, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilizindua Mwongozo wa Kitaifa wa AI katika Elimu pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa matumizi ya Kidijitali katika Elimu 2024/25–2029/30. Kupitia utekelezaji wa mikakati hiyo, walimu 1900 wa shule za sekondari wamepatiwa mafunzo kuhusu matumizi ya Akili Unde katika mfumo mzima wa ufundishaji na Ujifunzaji.
Mifumo mbalimbali ya Akili Unde imeanza kutumika katika shule, vyuo vya ualimu, taasisi za elimubya Ufundi na vyuo vikuu, kwa lengo la kuboresha ufundishaji, ujifunzaji, utafiti na ubunifu.
Tanzania imekwenda katika mkutano huu ikiwa na ujumbe kuwa Akili Unde inapaswa kutumika kwa manufaa chanya kwa kuwa chachu ya ujumuishi, kuhamasisha ujifunzaji endelefu, kuchochea fikra tunduizi na ubunifu katika Elimu