
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi amesema kuwa matumizi ya sayansi, ubunifu na teknolojia ni nguzo muhimu katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii nchini.

Akizungumza Aprili 1, 2026 katika ufunguzi rasmi wa Mkutano wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Jarida la Tanzania Journal of Science (TJS) uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Mushi alisema kuwa sayansi imeendelea kuwa chombo muhimu cha kuendesha maendeleo kwa kuchochea ubunifu, kusaidia utungaji wa sera na kuimarisha sekta mbalimbali za uzalishaji.

Alisema kuwa kwa kipindi cha miaka 50, jarida hilo limekuwa jukwaa muhimu la kusambaza tafiti za kisayansi zenye ubora, hivyo kuchangia maendeleo ya taifa na kuongeza mchango wa Tanzania katika maarifa ya kisayansi duniani.

Prof. Mushi alieleza kuwa kaulimbiu ya mkutano huo inayohusu mustakabali wa sayansi asilia na tumizi katika maendeleo ya viwanda na jamii ni ya wakati muafaka, hasa ikizingatiwa dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2050 (TDV 2050), ambayo inategemea kwa kiasi kikubwa matumizi ya tafiti, ubunifu na teknolojia katika kukuza uchumi, kulinda mazingira, kuimarisha usalama wa chakula na mifumo ya afya.

Aidha, alibainisha kuwa mkutano huo umeleta pamoja wadau mbalimbali wakiwemo watafiti, watunga sera, sekta binafsi na washirika wa maendeleo, jambo linaloonyesha umuhimu wa ushirikiano katika kutatua changamoto za maendeleo


