
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, Januari 5, 2026 jijini Dodoma, amekabidhi magari manne yenye thamani ya Sh. milioni 904.84 kwa Wathibiti Ubora wa Shule nchini. Hatua hii inalenga kuwawezesha kufuatilia na kuimarisha huduma za utoaji wa elimu bora kwa wote, ikiwemo watoto wenye mahitaji maalum.

Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, Prof. Mkenda amesema kuwa Wathibiti Ubora wa Shule ni mboni ya Serikali katika sekta ya elimu, hivyo amewasisitiza kuwa mstari wa mbele kubaini changamoto na kuziwasilisha mapema sehemu husika ili kushughulikiwa. Aidha, amewataka kutembelea kaya kwa kaya ili kuwabaini watoto wenye ulemavu na kuhakikisha wanaandikishwa shuleni.

Waziri huyo amewapongeza Viongozi wote na Watendaji wa Wizara kwa utekelezaji wa mageuzi ya elimu kwa ufanisi, huku akisisitiza kuongeza kasi ya utekelezaji ili kufika azma ya Serikali ya utoaji elimu bora na jumuishi kwa makundi yote.

Amewashukuru wadau wote wa elimu kwa kuendelea kushirikiana na Serikali, na kwamba ushirikiano huo uendelea katika utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo kwa manufaa ya Taifa.

