Mkurugenzi wa Elimu Maalum, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Magreth Matonya, amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji kwa walimu wenye uhitaji maalumu nchini.



Akizungumza katika hafla ya uzinduzi na ugawaji wa Magari kwa Wathibiti Ubora wa Shule na vifaa vya TEAHAMA na saidizi Januari 5, 2026 jijini Dodoma, Dkt. Matonya amesema kuwa, kati ya vifaa vilivyozinduliwa, asilimia 90 ni vya kidijitali, hivyo vitawasaidia walimu, wakufunzi na walimu tarajali katika kuboresha mbinu za ufundishaji na kuongeza ufanisi wa utoaji wa elimu.



“Tathimini yetu ilibaini walimu 1,055 wanakabiliwa na changamoto za ufundishaji. Miongoni mwao, walimu 342 wenye ulemavu wa viungo hawana vifaa vya kufundishia, walimu 310 wenye ulemavu wa uoni, viziwi, wenye ualbino na wale wenye matatizo ya usikivu,” amesema Dkt. Matonya.