Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amewaaga vijana 16 watakaokwenda kusomea masomo ya sayansi na teknolojia katika Chuo Kikuu cha Johannesburg, Afrika Kusini kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended.



Akizungumza Januari 30, 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla hiyo, Prof. Mkenda amesisitiza kuwa mpango huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza idadi ya wataalamu wa sayansi na teknolojia nchini, hususan katika nyanja za Data Science, Akili Unde na Allied Sciences.



Mpango wa Samia Scholarship Extended unalenga kutoa fursa kwa wanafunzi bora wa Kitanzania waliopata ufaulu wa juu katika Kidato cha Sita, hasa kwenye masomo ya sayansi ikiwemo Advanced Mathematics.



Prof. Mkenda amesema wanufaika wote 50 wanatoka shule mbalimbali za kata, serikali na binafsi, jambo linaloonyesha kuwa fursa hii inatolewa kwa wote wenye uwezo bila kujali asili ya shule au familia.



Ameongeza kuwa Baada ya kundi la kwanza, serikali imepanga kupeleka wanafunzi wengine 34 katika vyuo vya kimataifa vilivyoko Ireland Kaskazini.