
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Tanzania ipo katika mageuzi makubwa ya elimu yanayolenga kuwawezesha vijana kupata ujuzi na stadi zinazokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Waziri Mkenda ameeleza hayo Machi 25, 2026 jijini Dar es Salaam katika Kongamano la Kimataifa la Maboresho ya Sera ya Elimu na Mitaala, ambapo amesisitiza kuwa ajenda ya mageuzi hayo ni kipaumbele cha taifa kisichoweza kupuuzwa wala kuahirishwa.

Prof. Mkenda amesema mageuzi hayo yalianza kutekelezwa hatua kwa hatua, ambapo mitaala mipya ilianza kutumika kuanzia Elimu ya Awali hadi darasa la tatu, huku darasa ya nne hadi saba likiendelea na mtaala wa zamani.

Amebainisha kuwa, walioanza na mtaala mpya wakiwa darasa la tatu, watakapofika darasa la sita mwaka 2027 watakuwa wamemaliza elimu yao ya msingi hivyo kifanya mwaka kiwa na madarasa mawili yanayomaliza elimu ya msingi.

Aidha, amesisitiza kuwa utekelezaji wa mageuzi hayo unahitaji ushirikiano wa wadau wote, akieleza kuwa, tayari Waziri Mkuu alitoa maagizo kwa Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule ya sekondari inayofikiwa na wanafunzi kwa urahisi ifikapo mwaka 2028.


