Serikali imejipanga kuongeza wataalam katika eneo la teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na Akili unde kwa kusomesha watanzania nje ya nchi na kuongeza miundombinu na vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia katika eneo hilo.



Akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 16, 2026 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo katika Mradi wa kuboresha miundo mbinu katika Ndaki ya TEHAMA ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof. Adolf Mkenda amesema juhudi hizi zinatokana na maono ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza wataalam katika eneo hilo kukidhi mahitaji ya Taifa katika eneo la teknolojia na Ubunifu.



Amesema tayari Serikali kupita Samia Scholarship imepeleka wanafunzi katika Vyuo vikuu mahiri nchini Afrika ya Kusini na Ireland kusoma katika eneo la Akili Unde, Sayansi ya Data na Sayansi Shirikishi ikiwa ni utekelezaji mkakati huo.



"Pamoja na kupeleka wanafunzi kusoma nje tuna chuo cha Indian Institute of Technology Zanzibar ambapo tunapelekea wanafunzi wa eneo hilo ngazi ya uzamili," amesema Prof Mkenda



Amewataka vijana kuona fursa kubwa zinakuja kupitia maendeleo na mabadiliko ya Teknolojia zinazotoa fursa ya ajira huku akisisitiza matumizi sahihi na salama ya Teknolojia.



Akizungumzia Ujenzi wa miundo mbinu unaofanywa na Serikali katika Ndaki ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waziri Mkenda amesema utaongeza udahili wa wanafunzi 351 pindi utakapokamilika, umetoa ajira 529 ambazo ni kwa wanataaluma na za muda mfupi.