
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI wameanza kutoa mafunzo ya Ufungamanishaji wa Mfumo wa Usimamizi wa Kujifunza (LMS) na Darasa Janja (Smart Class) kwa viongozi wa mikoa, halmashauri, kata na walimu nchini, yakiwa na lengo la kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa njia ya kidigitali.
Mafunzo hayo ya siku tano yameanza Agosti 11, 2025 Jijini Arusha, chini ya ufadhili wa Serikali kupitia mradi wa GPE-TSP yakilenga kuboresha mazingira ya ufundishaji kwa walimu. Ambapo Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) inashiriki kikamilifu katika maandalizi ya maudhui ya kidigitali na miongozo ya kitaaluma, kuhakikisha walimu wanapata nyenzo bora za kufundishia kupitia LMS na Darasa Janja.
Wanufaika ni pamoja na Maafisa Elimu Mkoa, Maafisa Elimu Sekondari, Wathibiti Ubora wa Shule, Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule pamoja na walimu wa TEHAMA, Hisabati, Fizikia, Kemia, na Baolojia.
Katika majaribio ya awali, shule nane kutoka mikoa mbalimbali zimechaguliwa kushiriki, ikiwemo Arusha (Arusha Jiji), Magamba (Lushoto DC, Tanga), Mabatini (Njombe Mjini), Dkt. Samia (Dodoma Jiji), Kalebezo (Buchosa DC, Mwanza), Udzungwa (Kilolo DC, Iringa) na Tumekuja (Unguja Mjini, Zanzibar).