Serikali ya Tanzania imeendelea kutekeleza kwa kasi mageuzi ya elimu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 sambamba na mwelekeo wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Mageuzi haya yanalenga kuimarisha ujuzi, sambamba na matumizi ya sayansi na teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji.



Akizungumza Agosti 18, 2025 Jijini Dodoma katika kikao na ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Bi. Muna Meky Meneja wa Programu za Elimu kwa Afrika Mashariki, Katibu Mkuu wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa mafanikio ya utekelezaji wa sera hiyo yanatokana na msaada wa kiufundi kutoka kwa Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo.



“Kwa msaada wa wadau wetu, tumeanza kujenga msingi imara wa namna ya kuimarisha ujuzi wa karne ya 21. Tunahitaji kuongeza matumizi ya TEHAMA katika kufundishia na kujifunzia ili kuendana na mahitaji ya sasa ya dunia ya kidijitali,” amesema Prof. Nombo.



Aidha, Prof. Nombo ameeleza kuwa Serikali itakikisha inatekeleza elimu ya lazima ya miaka 10, kuimarisha mafunzo ya walimu, pamoja na kuboresha elimu ya amali ili kuwajengea vijana maarifa, ujuzi na ubunifu unaohitajika katika soko la ajira kimataifa.



Kwa upande wake Bi. Muna Mecky kutoka Benkinya Dunia amesifu juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutekeleza miradi inayofadhiliwa na Benki hiyo, amesema kuwa Tanzania ina programu za elimu zilizo pana na zenye mafanikio makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.



Katika mazungumzo yake, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza kwenye elimu ya msingi na kuhimiza matumizi ya mifumo jumuishi ya ufadhili kama vile Multi-Programmatic Approach (MPA), ambayo hutoa fursa ya kushirikisha rasilimali za kikanda na kimataifa. Alieleza kuwa Benki ya Dunia iko tayari kushirikiana na Serikali katika kupanga vipaumbele vya ufadhili kwa miaka ijayo