Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, leo Agosti 15, 2025, ameshiriki katika semina maalum ya kuwaaga Watanzania 10 waliopata ufadhili wa masomo ya Shahada za umahiri (Masters) kutoka Serikali ya Ireland kupitia Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.



Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mushi alisema Serikali ya Tanzania inaendelea kufanya juhudi kuhakikisha vijana wanapata fursa za kupata elimu na ujuzi unaohitajika katika ulimwengu sasa.



“Tunaishi katika dunia inayobadilika kwa kasi kubwa. Hatuwezi kubaki nyuma kama watazamaji; tunapaswa kuandaa nguvu kazi yetu ili iweze kuendana na kasi ya mabadiliko hayo,” alisema Prof. Mushi.



Aidha, aliwasihi wanufaika hao kutumia kikamilifu nafasi waliyoipata kwa kufuata ubora wa kitaaluma na kuhakikisha wanarejea nyumbani wakiwa na maarifa na ujuzi utakaosaidia kuchangia moja kwa moja katika maendeleo ya taifa.



Kwa upande wake, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Bi. Nicola Brennan, aliwapongeza kwa kufaulu mchakato wa ushindani mkali, akieleza kuwa ambapo waombaji walikuwa wengi na Watanzania 10 walibuka washindi.



“Tunajivunia sana nyinyi kwa kupata fursa hii. Hakikisheni safari hii inakuwa na maana kwa kuleta ujuzi na maarifa ambayo yanatarajiwa katika maeneo mnayokwenda kusomea”



Miongoni mwa fani ambazo wanafaika hao watazisomea ni shahada ya umahiri kwenye Data Science and Analytics, Architecture, Urbanism & Climate Action, Work and Organisational Behaviour, Global Health, Public Health, International Development, Data Analytics, Sustainable Finance na Robotics and Intelligent Manufacturing