Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa mageuzi ya elimu ni muhimu sana kwa taifa, hivyo tunalazimika kuyatekeleza ili kuandaa vijana wetu kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kutumia fursa za teknolojia kuleta maendeleo nyanja mbalimbali Nchini.



Prof. Mkenda amesema hayo Novemba 27, 2025 jijini Dodoma akifunga Mkutano wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (TAPSHA), akisisitiza kuwa katika moyo wa mageuzi ya elimu, ni muhimu kuwandaa vijana wetu ili waendane na mabadiliko ya teknolojia na mazingira ya kidigitali.



"Ili kuwaandaa vijana kwa soko la ajira na kukabiliana na changamoto za utandawazi, tushirikiane kutekeleza mageuzi na tuwekeze kwenye sayansi na teknolojia" amesema Prof. Mkenda.



Waziri Mkenda amesema kuwa, katika kutekeleza Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, pamoja na mambo mengine Wizara inafanya maandalizi kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari hatua ya chini mwaka 2028.



Aidha amesema kuwa Serikali inatambua mchango wa TAPSHA katika maendeleo ya elimu, hivyo amesisitiza chombo hicho kulinda familia ya walimu. Aidha amewapongeza walimu wote Nchini kwa kazi nzuri wanaofanya.