Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa tathmini endelevu kama nyenzo muhimu ya kuimarisha ubora wa elimu msingi nchini, kwa lengo la kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi.



Akizungumza leo Aprili 16, 2026 jijini Dodoma katika hafla ya uwasilishaji wa taarifa ya tathmini ya ujifunzaji ngazi ya elimu msingi, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha sekta ya elimu, ikiwemo kuimarisha miundombinu ya shule ili kuinua mazingira bora ya kujifunzia.



“Serikali itaendelea kuimarisha tathmini endelevu kama msingi wa ubora wa elimu, sambamba na kuhakikisha shule zote zinakuwa na miundombinu bora na rasilimali za kutosha kwa ajili ya kufanikisha ufundishaji na ujifunzaji wenye tija,” amesema Mhe. Wanu.



Aidha, amesema Serikali itaongeza kasi ya uchapishaji na usambazaji wa vitabu vya kiada na ziada, pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau wa elimu, ili kuhakikisha malengo ya kuboresha elimu nchini yanafikiwa.



Hafla hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wa elimu, wakiwemo maafisa elimu, walimu na washirika wa maendeleo, kujadili hali ya elimu msingi, kubaini changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya maboresho.