Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Wanu Hafadh Ameir amesema kuwa ujenzi wa majengo mapya katika Kampasi ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kampasi ya Mizengo Pinda, mkoani Katavi ni hatua ya kimkakati katika kuongeza fursa za elimu ya juu na kuimarisha utafiti wa kilimo nchini.



Akizungumza Machi 14, 2026 Mkoani Katavi Mhe. Ameir amesema kuwa Kampasi hiyo itakuwa kitovu cha mafunzo na tafiti zitakazosaidia kuongeza tija ya kilimo na kuandaa wataalamu watakaowezesha taifa kujitegemea kiuchumi.



Naibu Waziri amesema kuwa Kampasi hiyo ni ushahidi wa dhamira thabiti ya Serikali ya kuwekeza katika sekta ya elimu na kuimarisha miundombinu ya vyuo vikuu.



Ameongeza kuwa Kampasi ya SUA Katavi inatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya mkoa huo kwa kutoa ajira, kuimarisha biashara ndogo ndogo, na kusaidia wakulima kupata maarifa ya kisayansi yatakayoongeza uzalishaji na thamani nmazao na kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Katavi na Taifa kwa ujumla.