
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameielekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na wadau wote kuhakikisha ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu Mzumbe katika eneo la Gombero wilayani Mkinga Mkoani Tanga unakamilika kwa wakati ili kuwezesha kuanza kwa mwaka mpya wa masomo Oktoba 2026.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kampasi hiyo Februari 15 2026, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa kasi ya ujenzi lazima iendane na malengo ya kitaifa ya kupeleka elimu ya juu na elimu ya ujuzi katika maeneo ya pembezoni, ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Waziri Mkuu Nchemba ametoa wito kwa wizara zote husika na Taasisi za kifedha kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha huduma za kijamii na miundombinu ya msingi zinapatikana ndani ya kampasi hiyo.

Akizungumzia Kampasi 16 za Vyuo Vikuu zinazojengwa katika mikoa 15 hapa nchini Waziri Mkuu Nchemba amesema zitasaidia kupokea idadi kubwa ya wanafunzi wanaohitimu sekondari kufuatia mafanikio ya mpango wa Elimu bila ada, sambamba na kuinua Uchumi wa maeneo husika na kuboresha miundombinu.

Ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu Mzumbe Mkoani Tanga unahusisha miundombinu ya madarasa ya kufundishia na kujifunzia, hosteli za wanafunzi, kituo cha afya, ukumbi wa chakula, nyumba za wafanyakazi na tenki kubwa la maji.


