
Kamishna wa Elimu Dkt Lyabwene Mtahabwa amesema kuwa mabadiliko katika elimu ni sawa na mabadiliko katika nchi, amesema hivyo akisisitiza dhamira ya Serikali kutekeleza kikamilifu Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 kwa ushirikiano na wadau ili kufanikisha azma ya kuwa na Mtazania mwenye maarifa, ujuzi na mzalendo.

Dkt. Mtahabwa ametoa kauli hiyo jijini Dodoma Aprili 15, 2026 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa mwaka wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali Tanzania (TAMONGSCO) akibainisha kuwa mageuzi ya elimu yanagusa maeneo makuu matatu ambayo ni kichwa kwa maana ya kuwapa wanafunzi maarifa, moyo ikilenga kukuza na kutunza maadili na utamaduni, huku mikono ikiwa kuwapatia wanafunzi ujuzi na stadi za kazi zitakazowawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na maendeleo.

Dkt Mtahabwa amesema Wizara imekuwa ikishirikiana na TAMONGSCO na wadu wengine wa elimu katika kupanga, kutekeleza, kubaini mapungufu na kutafuta suluhisho la changamoto zinazojitokeza.

“Kupitia ushirikano huu hakuna kitakachoshindikana na tuna imani imani ya kupata ushindi katika kuimarisha sekta ya elimu nchini,”amesisitiza Dkt. Mtahabwa.


