Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, Januari 26, 2026 jijini Dodoma, amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Elimu Matokeo, Bi. Rakshita Vaya, kwa lengo la kujadili maboresho ya mfumo wa elimu nchini.



Taasisi ya Elimu Matokeo inalenga kubadilisha mfumo wa elimu kwa kutoa programu bora, jumuishi na zinazopatikana kwa urahisi ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi wa ngazi mbalimbali pamoja na jamii kwa ujumla.



Katika kikao hicho, pande hizo mbili zimejadili mwongozo wa kitaaluma kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, utakaowawezesha kufanya machaguo sahihi ya mwelekeo wa taaluma na maamuzi ya baadaye kwa kutumia njia zisizo za kidijitali.



Vilevile, wamejadili umuhimu wa kutoa elimu ya ujuzi wa kifedha kwa wanafunzi kupitia njia za kidijitali na zisizo za kidijitali, ili kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha mapema.



Aidha, kikao hicho kimeangazia nyenzo za mafunzo endelevu kwa walimu, kwa kuzingatia matumizi ya uchambuzi wa data ili kuboresha upangaji na utekelezaji wa mafunzo hayo kulingana na mahitaji halisi ya walimu.