Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefanya Kikao cha 8 cha Kamati ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDC) Machi 31, 2026 jijini Dodoma katika Ofisi za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA).



Kikao hicho kiliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hussein Omar, ambapo wajumbe walijadili kwa kina masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha sekta ya elimu nchini.



Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ni pamoja na kuimarisha utayari wa sekta ya elimu kukabiliana na majanga, usimamizi wa hatari na mabadiliko ya tabianchi.



Aidha, kamati ilipokea na kujadili mwongozo wa kitaifa wa usambazaji wa vitabu vya kiada pamoja na mwongozo wa maendeleo endelevu ya kitaaluma kwa walimu unaotekelezwa kupitia shule na vituo vya rasilimali za walimu (TRC).



Katika hatua nyingine, kamati ilijadili utekelezaji wa mtaala mpya wa taifa kwa kuangalia utayari wa taasisi na mipango ya kimkakati, pamoja na maandalizi ya sekta binafsi kushiriki katika mpango wa wanafunzi wa mkupuo mara mbili (Double Cohort) unaotarajiwa mwaka 2028.



Vilevile, kikao kilijadili mkakati wa kitaifa wa kuhamasisha ushiriki wa Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora) katika maendeleo ya elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu.

-2026