
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za elimu kupitia uanzishaji wa maktaba za jamii nchini. Tarehe 2 Desemba 2025, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hussein Mohamed Omar, alizindua Maktaba ya Jamii ya Maguu, Mbinga kituo kitakachotoa huduma kwa wananchi wa rika zote kwa kujumuisha.

Dkt. Omar amesema maktaba hizo ni chachu ya kuongeza maarifa, ubunifu na elimu endelevu kuelekea kutimiza Dira 2050 na utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014 (toleo 2023). Amehimiza maktaba kutoa huduma bila ubaguzi na Serikali itaendelea kutenga fedha kuanzisha na kuboresha maktaba zenye vitabu, kompyuta na vifaa vya kujifunzia.

Mkurugenzi Mkuu wa TLSB, Dkt. Mboni Ruzegea amesema Maktaba ya Maguu ni ya 55 nchini na imeanzishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Maguu Community Based Information Centre Association (MACOBICA) ambapo serikali imetoa vitabu vyenye thamani zaidi ya Tzs milioni 10 ukarabati na samani, hivyo kuwa “Chuo cha wazi” kwa wananchi.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbinga, Bi. Pendo Ndumbaro, ameahidi kuhamasisha matumizi ya maktaba huku Mwenyekiti wa MACOBICA, Simon Mahai akibainisha kuwa maktaba inalenga kusaidia vijana na wanafunzi kuepuka vishawishi na kupata mazingira salama ya kujifunza na kujenga maisha bora.


