
Kituo cha Umahiri cha Nishati Jadidifu cha Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kilichopo katika Kampasi ya Kikuletwa, Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, kimekusudiwa kuwa kitovu cha mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa chuo hicho.

Kupitia ushirikiano wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Benki ya Dunia, katika kituo hicho unajengwa mtambo wa kufua umeme wa maji wenye uwezo wa kuzalisha megawati 1.6. Umeme huo unatarajiwa kutumika katika Wilaya ya Hai na kuchangia upatikanaji wa nishati safi kwa jamii.

Ujenzi wa mtambo huo umekamilika kwa asilimia 85.5 na umechangia kutoa ajira kwa zaidi ya watu 50 katika eneo la Wilaya ya Hai.

Aidha, mtambo huo umejengwa na kusimamiwa na walimu wa ATC, hatua ambayo imewawezesha kupata uzoefu wa moja kwa moja katika ujenzi wa miundombinu ya nishati safi.

Kituo hiki kinatarajiwa kuongeza ujuzi wa vitendo kwa wanafunzi wa fani hiyo na kuimarisha nafasi ya ATC kama chuo kinachoandaa wataalamu wa nishati jadidifu katika ukanda wa Afrika Mashariki.


