Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeeleza kuwa inaendelea kutekeleza ajenda yake ya kuifanya elimu ya juu nchini kuwa ya ushindani katika ngazi ya kimataifa kupitia utekelezaji mpango wa Umataifishaji. (Internationalization).



Kauli hiyo imetolewa tarehe 30 Septemba 2025, mjini Morogoro, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, wakati wa mazungumzo na Rais na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Simon Fraser (SFU) cha Canada, Dkt. Joy Johnson ambapo alieleza kuwa Serikali inaweka mkazo katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa kubadilishana wanafunzi na wahadhiri na kufanya tafiti za pamoja zitakazo wezesha kutatua changamoto za kidunia.



Aidha, Prof. Nombo alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua za kupata vifaa na mitambo ya kisasa ya kujifunzia na kufundishia, ili kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi stahiki katika ngazi zote za elimu.



Kwa upande wake, Dkt. Joy Johnson alieleza kuwa Chuo Kikuu cha Simon Fraser kinaunga mkono juhudi za Tanzania katika kuboresha sekta ya elimu, na kwamba kitaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania katika maeneo mbalimbali.



Dkt Johnson aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na utoaji wa fursa za mafunzo nchini Canada, ukuzaji wa biashara changa za wabunifu, mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa fani mbalimbali, pamoja na uanzishaji na uendelezaji wa vituo vya ubunifu.