Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, ameongoza Kikao cha Kamati Tendaji ya Kitaifa ya Usimamizi wa Utekelezaji wa Mradi wa EASTRIP kwa ajili ya kujadili maendeleo ya mradi huo pamoja na kuhakikisha maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia yanatekelezwa kwa wakati.



Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Desemba 16, 2025 jijini Mwanza, Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa tayari wamekutana na mkandarasi ili kusikiliza mpango wake wa kukamilisha kazi za ujenzi ifikapo Mei 2026, na kwamba Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa na Wilaya zitaendelea kufuatilia kwa karibu.



Kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DSM), Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), ujenzi wa miundombinu umekamilika isipokuwa Kituo cha Mafunzo ya Kuvuna Nishati Jadidifu cha ATC ambacho kimefikia asilimia 78.