
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi zote za dini ili kuhakikisha Elimu ya Dini inafundishwa ipasavyo na kuchangia katika kuhenga maadili mem kwa wanafunzi.

Akizungumza Januari 11, 2026 jijini Dar es Salaam, Prof. Mkenda amesema hayo baada ya kukabidhi nakala 5,000 za vitabu vya kiada vya Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa Kidato cha Pili pamoja na nakala 1,000 za vitabu vya Kiongozi cha Mwalimu kwa ajili ya shule zisizo za Serikali Nchini ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa somo hilo.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika uzalishaji wa vitabu vya masomo ya dini.

Amewahamasisha wanaosomea ualimu kuchukua masomo ya dini ili kuhakikisha upatikanaji wa walimu wa masomo hayo.

Kwa upande wake Mufti wa Tanzania Sheikh Dkt. Abubakar Ben Zuberi Bin Said Ally ameipongeza Serikali chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza mageuzi ya sekta ya elimu.

Naye, Mkurugenzi wa Elimu Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA) na Mweka Hazina wa Taasisi ya TISTA Mwl. Ali Ali ameishukuru Wizara ya Elimu, kwa kuzishirikisha taasisi za dini katika kutekeleza Sera ya Elimu na Mitaala iliyoboreshwa.


