
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema Vyuo Vikuu nchini ni nguzo muhimu ya maendeleo kwa kuendeleza maarifa kuchochea tafiti na ubunifu, na wataalamu wanaoweza kukabiliana na changamoto za karne ya 21.
Akifungua Mkutano wa Pili wa Kisayansi wa Muungano wa Vyuo Vikuu Vitano (5UC), Septemba 30, 2025 Mjini Morogoro, Prof. Nombo ametaja baadhi ya Vyuo hivyo ikiwemo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika (NM-AIST) na Chuo Kikuu cha Aga Khan kwamba vina mchango katika kuendeleza tafiti bunifu na programu za pamoja zinazolenga kutatua changamoto za kijamii na kimazingira.
Ametoa mfano wa Chuo cha SUA, akibainisha kuwa juhudi zake katika kilimo endelevu zimewezesha jamii kuhimili mabadiliko ya mazingira, na kuonyesha jinsi ushahidi wa kisayansi unavyoweza kubadili maisha ya watu kwa vitendo.
Aidha Prof. Nombo amesema tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1970, Tanzania imepiga hatua kubwa katika elimu ya juu, ikiwa na zaidi ya vyuo 50 vilivyodhinishwa na TCU hadi Julai 2025, hatua inayohakikisha ubora wa elimu na ushindani wa kimataifa.
Akigusia changamoto zinazokabili jamii, Prof. Nombo alitaja mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa chakula, mifumo dhaifu ya afya, na ukosefu wa usawa wa kijamii kama maeneo yanayohitaji ushirikiano wa kitaaluma. Alisisitiza kuwa janga la COVID-19 limetoa somo kuhusu umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya afya, na kwamba vyuo vikuu vina jukumu la kuongoza katika kujenga jamii jumuishi na zenye ustahimilivu.
Aidha, Prof. Nombo alitoa wito kwa washiriki wa mkutano huo unaohusisha wanazuoni, watunga sera, na wadau wa maendeleo kushiriki kikamilifu, kutoa mapendekezo ya sera, na kuendeleza ushirikiano wa utafiti unaoendana na ajenda za maendeleo za kitaifa na za kikanda kama Ajenda ya Afrika ya 2063. Alisisitiza kuwa elimu haina mipaka, na kwamba Tanzania iko tayari kuwa mshirika wa kuaminika katika kubadilishana maarifa duniani.