
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe, Wanu Hafidhi Ameir amesema Serikali inaendelea na mchakato wa kufanyia maboresho ya Sheria ya elimu ili iende sambamba na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023 pamoja na maboresho ya Mitaala.

Mhe. Wanu ameyasema hayo jijini Dar es salaam Februari 13, 2026 alipomuwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda katika kikao cha Wadau wa Mtandao wa Elimu (TEN/MET) kutoa maoni kwa ajili ya mapitio ya sheria ya elimu, sura ya 353.

Amesema Utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 unagusa ngazi zote za elimu na mafunzo hivyo, Wizara, pamoja na tathmini inayoendelea ya Sheria ya Elimu na sheria za Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara, inaendelea pia na mapitio ya miundo ya taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara kwa lengo la kuleta tija na ufanisi katika utekelezaji wa Sera.

“Sote tutakubaliana kuwa uwepo wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, Toleo la 2023 ni jambo moja, lakini utekelezaji wake unahitaji nyenzo mbalimbali za kuiwezesha kutekelezeka. Nyenzo mojawapo ni kuwepo kwa Sheria ya Elimu iliyoboreshwa hvyo tunawashukuru kwa kuendelea kutoa maoni ya kuboresha sharia yetu ya elimu,” amesema Mhe. Wanu.


