Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza kuanza kuratibu Asasi za Kiraia zinazotekeleza miradi ya elimu nchini, ili kupata taarifa sahihi kuhusu huduma wanazotoa na maeneo yanayonufaika, ili kuimarisha ushirikiano baina ya wadau wa elimu, kuongeza uwazi wa utekelezaji wa shughuli, na kuhakikisha kuwa rasilimali zinatumika kwa ufanisi zaidi katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.



Hatua hiyo imeelezwa Agosti 12, 2025 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, wakati wa kikao na Wajumbe kutoka Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), ambapo amesema kuwa itasaidia kuepusha kurudiarudia kwa shughuli zinazofanana katika eneo moja, hali inayoweza kusababisha matumizi yasiyo na tija ya rasilimali na kupunguza athari chanya kwa walengwa.



Kwa upande wake, Mratibu wa Taifa kutoka Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala, amesema kuwa mtandao huo umepata ufadhili kutoka MasterCard Foundation ya nchini Canada kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kutoa motisha kwa walimu. Mradi huo unalenga kuwajengea walimu uwezo kupitia mafunzo endelevu kazini, pamoja na kuwapatia vifaa na rasilimali muhimu kwa ajili ya vituo vya walimu. Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kufanyika katika mikoa 10 ya Tanzania Bara.



Bi. Makala ameongeza kuwa, ili kuhakikisha utekelezaji wenye tija na ushirikishwaji wa wadau wote muhimu, TEN/MET imeomba kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika kila hatua ya mradi. Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha uratibu wa shughuli, kuongeza uwazi, na kuhakikisha kuwa malengo ya mradi yanawafikia walimu kwa ufanisi katika maeneo husika.