Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Taasisi kutoka Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mh. Nolasco Jacob Kipanda, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amepongeza Wizara ya Elimu kwa kujielekeza kwenye matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kuboresha usimamizi wa rasilimali watu.



Mh.Kipanda ameyasema hayo Novemba 10,2025 mkoani Morogoro katika kikao kazi cha tathmini ya mahitaji ya rasilimali watu katika sekta ya elimu ambapo  amesema mfumo huo unasaidia kupata takwimu sahihi, hivyo kuwezesha maamuzi bora ya ajira, uhamisho na upangaji wa watumishi kwa ufanisi zaidi.



Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Edith Rwiza, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa upangaji wa watumishi wa sekta ya elimu unafanyika kwa haki, usawa na kwa kuzingatia mahitaji halisi ya vituo vya kazi kupitia mfumo wa *e-Msawazo*.



Ameongeza kuwa mfumo huo si tu unasaidia katika upangaji wa watumishi, bali pia ni nyenzo ya uwajibikaji na ufanisi katika matumizi ya rasilimali za umma.