
Serikali ya Tanzania inajivunia mafanikio ya Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP) uliotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Serikali ya Canada kupitia Global Affairs Canada (GAC).

Kauli hiyo imetolewa Aprili 9, 2026 na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, akieleza mafanikio na mipango ya uendelezaji wa mradi huo katika mkutano maalum na wadau kujadili mafanikio na uendelevu wa matokeo chanya ya mradi.

Amebainisha kuwa Serikali imetumia takriban Sh. bilioni 140 na Global Affairs Canada Sh. Bilioni 92 kuboresha miundombinu vifaa mifumo ya TEHAMA katika Vyuo 34 vya Ualimu.

"Tumejenga maabara, maktaba na kuongeza vitabu katika vyuo. Aidha vyuo vimeunganishwa na mfumo wa kimaktaba unaoitwa (COTUL), ambao umewezesha upatikanaji wa vitabu hivyo kuboresha mafunzo vyuoni," amesema Prof. nombo.

Ameongeza kuwa kupitia TESP vyuo vua Ualimu 25 vineunganishwa na Mkongo wa Taifa, hatua iliyowezesha matumizi ya mbinu na vifaa vya kidijitali katika ujifunzaji na ufundishaji.

Mradi huo ulizingatia ujumuishi na usawa wa kijinsia ili kuhakikisha fursa sawa katika mafunzo na uongozi.

Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Serikali kupitia mradi huu imejenga na kuboresha miundombinu kwa kuzingatia uhimilivu wa mazingira, na hivyo kutoa mfano wa ujenzi rafiki kwa mazingira.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa TESP imeacha alama kubwa, na Wizara kwa kushirikiana na vyuo vya ualimu imejipanga kuendeleza mafanikio hayo licha ya ushirikiano na Global Affairs Canada kufikia ukomo.


