
·Waazimia kukuza Matumizi ya Akili Unde (AI)
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameshiriki Kongamano la Nne (4) la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililofanyika kuanzia Machi 30 hadi Aprili 1, 2026 mjini Kigali, ambapo jumuiya hiyo ilitoa motisha ya kifedha kwa vijana wabunifu ili kuchochea matumizi ya teknolojia katika kutatua changamoto za kijamii.

Kupitia Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Baraza la Vyuo Vikuu la Afrika Mashariki na wadau wa maendeleo, wabunifu kutoka nchi wanachama walijishindia dola 10,000 kwa washindi wakuu na dola 1,400 kwa washindi wengine.

Akifunga kongamano hilo, Waziri wa Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Ubunifu wa Rwanda, Paula Ingabire, amesema ubunifu wa vijana umechangia sekta za elimu, kilimo, mazingira, afya na usafirishaji, huku akizitaka nchi wanachama kuongeza uwekezaji katika teknolojia hususan Akili Unde (AI).

Kongamano hilo pia lilipitisha maazimio 15 ya kukuza matumizi ya Akili Unde, yakilenga kuboresha sera, kuimarisha ujuzi, kuanzisha kituo cha kikanda cha teknolojia zinazoibukia na kuunda mfuko wa utafiti wa teknolojia hiyo.

Hatua hiyo inakuja wakati muafaka ambapo Tanzania kupitia mpango wa Samia Scholarship imeanza kuongeza uwekezaji katika maendeleo ya rasilimali watu kwenye teknolojia za kisasa, kwa kufadhili wanafunzi kusoma nje ya nchi katika fani za Akili Unde (AI), Sayansi ya Data, Uhandisi pamoja na Sayansi Shirikishi, hatua inayolenga kujenga wataalamu mahiri watakaosaidia kuharakisha mageuzi ya kidijitali na ubunifu nchini


