
Viijana 34 wanufaika wa Samia Scholarship Extended DS/SI + watanufaika na punguzo la ada ya masomo kwa asilimia 50 katika Chuo Kikuu cha Limerick cha Ireland, kufuatia makubaliano yaliyosainiwa Machi 26, 2026 jijini Dar es Salaam na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na chuo hicho.

Makubaliano hayo yamelenga kutoa fursa kwa vijana kusoma katika fani za Sayansi ya Data, Akili Unde na Sayansi Shirikishi. Wanafunzi hao ni miongoni mwa wanufaika 50 wa Mpango wa Ufadhili wa Samia Scholarship Extended DS/AI+.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema mpango huo wa kimkakati unalenga kuwawezesha vijana wenye vipaji kupata maarifa na ujuzi katika eneo teknolojia, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwana 2014 Toleo la 2023 inayosisitiza mafunzo katika sayansi na Teknolojia za sasa.

Kwa upande wake, Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan, ameipongeza Serikali kwa mpango huo wa kimkakati na kusisitiza kuwa vijana watarudi nchini wakiwa na ujuzi na uzoefu utakaochangia maendeleo ya sekta za teknolojia na ubunifu.

Naye, Makamu wa Rais wa Ushirikiano wa Kimataifa na Jamii wa Chuo Kikuu cha Limerick, Prof. Colin Fitzpatrick, amefurahia uwezo mkubwa walionao wanafunzi hao, ameahidi kuwa, kutokana mashirikiano ya chuo hicho na sekta za viwanda, wananafunzi hao watapata fursa ya mafunzo ya vitendo katika makampuni makubwa ya kimataifa ambayo yatawezesha kukuza ujuzi na kuongeza ushindani wao sokoni.


