Katika jitihada za kuimarisha mfumo wa utafiti na ubunifu nchini Tanzania, ujumbe wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WyEST) ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Prof. Daniel Mushi, umefanya ziara ya kimkakati nchini Korea Kusini mnamo tarehe 25 Machi, 2026.



​Ziara hiyo, iliyoshirikisha pia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), imelenga kujifunza namna Korea Kusini ilivyoweza kupiga hatua kubwa ya viwanda kupitia usimamizi madhubuti wa Miliki Bunifu (Intellectual Property) na tafiti zinazolenga kutatua changamoto za moja kwa moja za viwanda.



​Moja ya maeneo yaliyovutia zaidi ujumbe huo ni mfumo wa kisasa wa Korea Kusini wa kuthamanisha Hataza (Patents) tofauti na mifumo mingi ambapo hataza hubaki kama sifa ya kitaaluma pekee, Korea imefanikiwa kutumia hataza kama dhamana ya kupata mikopo benki.



Pia imewawezesha wabunifu kupata mitaji ya ubiasharishaji wa teknolojia zao, kuchochea uzalishaji wa teknolojia kwa kiwango kikubwa (mass production) kupitia uwekezaji huo na kupunguza utegemezi wa teknolojia.

​Ujumbe huo pia ulitembelea Taasisi ya Sayansi ya Msingi ya Korea (KBSI) na taasisi nyingine za Utafiti na Maendeleo (R&D) kujifunza mikakati inayotumika nchini humo katika kupunguza utegemezi wa teknolojia kutoka nje kwa kuimarisha uwezo wa ndani wa uvumbuzi.