Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema suala la utekelezaji wa mabadiliko na maboresho yaliyofanyika kwenye Sera ya Elimu na Mafunzo, na Mitaala linahitaji ushirikiano wa hali ya juu miongoni mwa wadau wote wa elimu, taasisi za serikali na zile zisizo za serikali, wazazi na jamii yote kwa ujumla



Makamu wa Rais amesema hayo, wakati akifungua Kongamano la Kimataifa kuhusu maboresho ya sera ya elimu na mitaala nchini, linalofanyika katika Ukumbi wa Maktaba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jijini Dar es Salaam. Ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Taasisi za elimu, hususan Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuendelea kufanya ufuatiliaji na tafiti ili kubaini dosari zozote zinazoweza kukwamisha utekelezaji wa suala hilo ili kubaini na kuibua maeneo yanayohitaji maboresho zaidi kiutendaji.



Makamu wa Rais, amesema suala la utekelezaji wa mabadiliko na maboresho yaliyofanyika kwenye Sera yetu ya Elimu na Mafunzo, na Mitaala kuanzia Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari hadi Elimu ya Juu. linataka Watanzania wote kutafsiri vema maono ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya mfumo wa elimu unaozingatia kutoa ujuzi na maarifa ili kumwezesha mhitimu kumudu mazingira yake, na kumudu ushindani kwenye ulimwengu wa kazi.



Aidha, Makamu wa Rais amesema suala la elimu jumuishi inayozingatia usawa ni miongoni mwa vipaumbele, ambapo Serikali imeweka msisitizo katika uwepo wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na miundombinu rafiki kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum. Amesema suala hilo linakwenda sambamba na uandaaji wa walimu wenye ujuzi wa elimu maalum ili kufundisha wanafunzi hao.



Maboresho yaliyofanywa na serikali kwenye baadhi ya maeneo ya Sera ya Elimu na Mafunzo, yamefanyika ili kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiikabili elimu ya Tanzania, zikiwemo, kujikita zaidi kwenye elimu ya nadharia badala ya vitendo na pia, kutokuwepo kwa fursa za elimu na mafunzo zinazozingatia mahitaji ya soko la ajira. Vilevile, mapungufu katika njia za ujifunzaji ambazo hazikukidhi hali halisi ya mazingira na maadili ya Kitanzania