
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo mapya ya Kampasi ya Mizengo Pinda ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), iliyopo katika Halmashauri ya Mpimbwe, Wilaya ya Mlele mkoani Katavi. Kampasi hii imekuwa chachu ya maendeleo ya elimu na fursa kwa vijana wa eneo hili na taifa kwa ujumla tangu kuanzishwa kwake mwaka 2019.

Majengo hayo ni pamoja na jengo la taaluma lenye uwezo wa kuchukua Wanafunzi zaidi ya 2000 pamoja na bweni litakalokuwa na uwezo wa kuchukua Wanafunzi 400 ambapo yanajengwa na Serikali kupitia Mradi wa Elimu ya Juu Kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 17

Kampasi ya Mizengo Pinda inatoa programu tatu za masomo ambazo ni Shahada, Stashahada, na Astashahada. Programu hizi zimejikita katika kilimo, ufugaji, utalii, na uhifadhi wa wanyamapori, zikilenga kuendeleza ujuzi wa vitendo na kuchochea shughuli za kiuchumi zinazohusiana moja kwa moja na mazingira ya Katavi.


